NIPASHE
Mgombea wa kiti cha urais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) na Waziri wa
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe ‘amefunguka’
baada ya kupenya katika kundi la tano bora, akisema iwapo wajumbe wa
Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), hawatamuunga mkono, yupo tayari
kuheshimu maamuzi yao.
Membe na makada wenzake, Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Asha Rose Migiro, Naibu Waziri wa Sayansi, Mawasiliano na Teknolojia, January Makamba, Balozi wa Kudumu wa Umoja wa Afrika (AU), nchini Marekani, Amina Salum Ali,
ndio waliopeta kati ya wagombea 38 waliorejesha fomu, wakiomba
kuteuliwa na chama hicho kupeperusha bendera katika uchaguzi mkuu wa
Oktoba 25, mwaka huu.
“Hata
kama sitachaguliwa na wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa, kuwa mgombea wa
CCM katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu, nitamuunga mkono
atakayechaguliwa. Kukubali kushindwa ni sehemu ya demokrasia na mimi
nimejiandaa kisaikolojia kupokea matokeo yoyote…Lakini pia niwapongeze
wote waliofika tano bora,” Membe.
Mgombea mwingine, Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli
alipoulizwa kuhusu mapendekezo ya Kamati Kuu (CC) kuliteua jina lake
kuwa miongoni mwa majina matano yatakayopigiwa kura ili kupata majina
matatu yatakayopigiwa kura ili kumpata mgombea mmoja atakayepeperusha
bendera yake dhidi ya vyama vya upinzani, alikataa kuzungumza huku
akiwapungia mkono wananchi waliojitokeza eneo hilo.
Naye, Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Asha-rose Migiro akizungumzia
mchakato huo namna ulivyokwenda licha ya kuwapo kwa mpasuko kati ya
baadhi ya wajumbe wa Kamati Kuu ambao wanapinga maamuzi ya kuminya
wagombea wanaokubalika ndani na nje ya CCM akiwamo Lowassa, Migiro
alisema kitendo cha kuaminiwa na CCM, hadi kufika hatua ya tano bora,
ni unyenyekevu uliopitiliza ambao unapaswa kuheshimiwa.”
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Sayansi, Mawasilino na Teknolojia,
January Makamba, alisema “Tayari chama changu kinaamini kuwa mimi
ninaweza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania…kwa hiyo kwangu
mimi ni heshima kubwa sana.”
Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja ambaye ni miongoni mwa wagombea
walioshindwa kupenya tabo bora, alisema kuwa kilichofanywa na Kamati Kuu
ya CCM; ni utaratibu wa kawaida ambao vyama vilivyokomaa kidemokrasia
vimekuwa vikiufuata.
“Mimi
binafsi naafiki kuwa kilichofanyika ni utaratibu wa kawaida ambao
hufuatwa na chama change. Wametenda haki wajumbe wa Kamati Kuu lakini
pia nakubaliana nao kwamba, wagombea wote waliochaguliwa wana uwezo wa
kuliongoza taifa hivyo sina wasiwasi nao,”
NIPASHE
Watu wasiofahamika wamesambaza
vipeperushi Zanzibar kupinga maamuzi ya Kamati Kuu ya CCM kuwakataa
wanasiasa wakongwe waliojitokeza kuwania nafasi ya urais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania akiwemo Makamu wa Rais, Dk. Mohammed Gharib Bilali na Waziri mkuu wa zamani Edward Lowassa.
Vipeperushi hivyo vyenye kurasa mbili
vimeonekana katika maeneo tofauti vikiwa na kichwa cha habari “Sauti ya
salama Zanzibar”, vimeeleza kuwa kutokana na maamuzi hayo wanachama wa
CCM wa kundi la sauti ya salama kuanzia leo ndio mwisho wa wanachama wa
sauti ya salama kuendelea kubakia ndani ya CCM.
Walisema kundi hilo linaundwa na mikoa
sita ya kichama, wamefikia uamuzi huo baada ya kuridhishwa na utaratibu
mzima wa upatikanaji wa mgombea wa nafasi ya urais kutokana na chama
kushindwa kupitisha mgombea ambaye ni chaguo la wananchi na wanachama.
“Kama
mtatuletea mgombea wenu wa mfukoni badala ya Lowassa ambaye ndio chaguo
la wanachama wengi na wananchi, Jumapili ndio mwisho kwa wanachama wa
sauti ya salama kuendelea kubakia ndani ya CCM”, vimeonya vipeperushi hivyo.
Aidha, kundi hilo limesema wajumbe wa
halmashauri kuu ndio wanaowategemewa na kama watashindwa kukiokoa chama
kwa kushindwa kuwapatia wanachotaka, wanachama historia itakuja
kuwahukumu kama ilivyotokea kwa vyama vya ukombozi katika mataifa ya
Malawi, Zambia na Kenya baada ya vyama husika kushindwa kuheshimu
demokrasia ya ndani ya chama.
Kundi hilo limesema kuwa kumbukumbu
inaonyesha mchakato wa kupata mgombea wa urais CCM umekuwa ukimalizika
na kuacha nyufa ndani ya chama kama ilivyotokea mwaka 2000 baada ya
wananchama na wananchi wa Zanzibar kumtaka aliyekuwa Waziri Kiongozi,
Dk. Mohammed Gharibu Bilali awe mrithi wa rais mstaafu Dk Salmin Amour,
baada ya kumaliza muda wake.
Vipeperushi hivyo ambavyo vimeibua
mjadala vimeeleza kwamba mwaka 2010 chama kiliendelea kurejea makosa
yale yale kuchagua mgombea wa mfukoni badala ya yule aliyetakiwa na
wananchi ambao walikuwa wakimtaka Dk. Bilal na badala yake aliletwa
mgombea Dk Ali Mohammed Shein na kusababisha CCM kushinda kwa asilimia
51.
“Kamati kuu, halmashauri kuu pamoja na
mkutano mkuu kama utashindwa kusoma alama za nyakati tutalazimika
wanachama kupita njia yenye usalama na miguu yetu, kumbukeni vipo vyama
vingi na tayari Chadema imetuonesha njia”.
Hata hivyo wasemaji wa CCM hawakuweza
kupatikana kutokana na kuhudhuria vikao vya chama Dodoma akiwemo Naibu
Katibu mkuu wa CCM, Vuai Ali Vuai, lakini Kamanda wa polisi mkoa wa
mjini Magharibi Mkadam Khamis Mkadam, alisema hadi jana hajapokea
taarifa ya kusambazwa vipeperushi vinavyopinga maamuzi yanayoendelea
kutumika ya kupata mgombea wa urais.
NIPASHE
Wachambuzi wa masuala ya kisiasa
wamesema kuwa kitendo cha makada watatu wa Chama cha Mapinduzi (CCM),
Mjumbe wa Kamati Kuu, Dk. Emmanuel Nchimbi, Sophia Simba na Adamu
Kimbisa, kueleza kuwa, hawakubaliani na maamuzi yaliyofanywa na Kamati
Kuu ni kiashirio kuwa, CCM imeyumba na inampasuko ndani yake.
Mchambuzi wa Siasa na Uongozi,
Rutashobya Rutashobya, akizungumza na NIPASHE Jumapili jana alisema kuwa
kitendo cha makada hao juzi usiku kuibuka na kauli moja kuwa,
hawakubaliani na maamuzi yaliyofanyika maana yake wamekosa umuvilivu wa
kisiasa na kusababisha chama kuyumba.
Juzi makada hao baada ya kumalizika kwa
kikao cha Kamati Kuu, waliwaeleza waandishi wa habari kuwa,
hawakubaliani na maamuzi yaliyofanywa na kikao hicho ya kuminya baadhi
ya majina ya wagombea.
Aidha, walisema kuwa wameletewa majina
machache yaliyojadiliwa na Kamati ya Maadili, kitendo ambacho
hawakukubaliana nacho kwa mujibu wa Katiba ya chama.
Nchimbi na wenzake walisema tayari
wameshawataarifu wenzao kuhusiana na maamuzi yaliyofanywa na Kamati Kuu
ya kutounga mkono kile kilichotokea.
Akizungumzia maamuzi hayo, Rutashobya,
alisema , makada hao walitakiwa kuwa na uvumilivu wa kisiasa lakini
walichokifanya inaonyesha dhahiri kuwa kuna mpasuko na chama kimeyumba.
Aidha, alisema kwa wale walioenguliwa
kwa bahati mbaya sababu hazijawekwa wazi hivyo ni vigumu kama wachambuzi
kuchambua kitaalam.
Aidha alisema bado wananchi wana nafasi kubwa ya kuchagua Rais ajae.
Akielezea kuhusu kuenguliwa kwa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, ambaye mikutano yake wakati akitafuta udhamini ilifurika wananchi, alisema inawezekana waliokuwa wakijitokeza walikuwa wanapenda kitu kingine cha ziada na sio mhusika.
Akielezea kuhusu kuenguliwa kwa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, ambaye mikutano yake wakati akitafuta udhamini ilifurika wananchi, alisema inawezekana waliokuwa wakijitokeza walikuwa wanapenda kitu kingine cha ziada na sio mhusika.
“Mtu aliyekuwa anajaza umati mkubwa
uwanjani leo ameenguliwa lakini nchi ipo shwari hakuna aliyeenda
barabarani kufanya maandamano kupinga maamuzi, ni tafsiri kuwa labda
umati ule ulikuwa ukienda pale kushangaa waimbaji, magari na sio upendo
wa dhati kwa mhusika,” alisema.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam
(UDSM) Bashiru Ally, alisema kama mchambuzi wa siasa, kilichotokea na
kitachotokea atakichambua kwa kina kwa faida ya Watanzania.
Alisema endapo leo jina la mgombea
litatoka basi atakuwa na uwanja mpana wa kuchambua mchakato mzima kutoka
watia nia 42 hadi wakabaki 38 na mwishoe watano.
Kuhusu kuenguliwa kwa Lowassa na watia
nia wengine alisema anaamini maswali yanayoulizwa nje na wananchi hata
ndani ya vikao yapo.
“Huu ni mwanzo tu kwa yaliyotokea
nafikiri yapo matokeo kama 1000 yataweza kutokea lakini sasa ni mapema
mno kuchambua tuvute subira hadi jina la mgombea urais litakapotoka,”
alisema.
Mhadhiri Mwandamizi wa Idara ya Sayansi
ya Siasa na Utawala wa Umma, Alexander Makulilo, alisema kilichotokea
kwa CCM inaonyesha kuwa, kuna shida labda Kamati ya Maadili ilipeleka
Kamati Kuu majina kama muhuri wa kupitishwa majina badala ya kufanyiwa
kazi.
Akitoa maoni kuhusu tano bora, alisema miongoni mwao atakayechaguliwa akipata mfumo mzuri wa uongozi mambo yataenda vizuri.
Mhadhiri wa Chuo kikuu cha Dar es
Salaam, Dk. Benson Bana, alisema kuenguliwa kwa mtu ambaye alikuwa
anaonekana ana nguvu kubwa kwa wananchi ni kiashirio tosha kuwa kazi
ndani ya CCM haikufanyika kwa vigezo.
kadhalika kuhusu kitendo cha baadhi ya
makada kutangaza kuwa hawana imani na kilichotokea, alisema “Hata kama
walifanya mchujo huu naamini CCM ina watu wenye busara na hekima kwa
hiyo walipaswa kuwa na maridhiano,” alisema.
Aliongeza kuwa kiashiria cha
kilichotokea ni kwamba uchaguzi mkuu utakuwa na makundi yanayopingana
ndani ya chama na kuleta fursa kwa upinzani.
Alisema kuwa inapotokea chama kinamkataa mgombea mwenye watu wengi nje anaweza kwenda upinzani na kuzigawa kura.
Aidha, alikitaka chama tawala kujitathmini upya kupitia kile kilichotokea cha baadhi ya wajumbe kupinga maamuzi.
“CCM iangalie upya kanuni zake ili hapo baadaye watu waweze kuhoji maamuzi inapobidi,” alisema.
MWANANCHI
Sasa ni wazi; mmoja kati ya Dk John
Magufuli, Dk Asha Rose Migiro au Balozi Amina Salum Ali atapeperusha
bendera ya CCM kwenye Uchaguzi Mkuu ujao baada ya wajumbe wa Mkutano
Mkuu kukamilisha kazi yao ya kupiga kura usiku mwingi wa kumkia leo.
Licha ya mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya
Kikwete kutangaza kuwa matokeo ya kura hizo yatatangazwa leo saa 4:00
asubuhi kuna kila dalili kuwa Waziri wa Ujenzi, Dk Magufuli ndiye
atakayepeperusha bendera ya chama hicho.
Lakini ushindi wa Dk Magufuli unakabiliwa kikwazo kikubwa kutoka kwa makada hao wawili wanawake na wanadiplomasia.
Watatu hao walifanikiwa kuingia hatua
hiyo ya mwisho ya kupigiwa kura na mkutano mkuu baada ya kuwabwaga
makada wengine wawili, Bernard Membe, ambaye alikuwa akipewa nafasi
kubwa kutokana na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kuenguliwa na
Kamati Kuu juzi, na January Makamba katika kura zilizopigwa na wajumbe
wa Halmashauri Kuu.
Awali kabla ya kupigiwa kura na Mkutano
Mkuu jana, Kikwete aliwataka wajumbe kumuunga mkono mgombea
atakayepitishwa kupeperusha bendera ya chama hicho na kuachana na
makundi.
“Wagombea wapo watatu na wote wana sifa
za kuwa Rais. Halmashauri Kuu imewapitisha kwa kujiridhisha na tabia na
mienendo yao na atakayepitishwa ataiongoza nchi yetu vizuri. Anatakiwa
apatikane Rais zaidi yangu ili tusonge mbele. Tunataka rais atakayefanya
mambo zaidi yangu,” alisema JK.
“Tumevuka hatua ya makundi na sasa
tunatafuta mgombea wa chama na si mgombea wa kundi au mgombea binafsi.
Wagombea urais waliojitokeza walikuwa 38 na makundi lazima yalikuwa
mengi. Tukipata mgombea mmoja makundi yanatakiwa kuyeyuka.”
Hisia za wajumbe kwa Dk Magufuli
zilionekana wazi wakati makada hao walipopewa dakika 15 za kujieleza
mbele ya Mkutano Mkuu, huku mwenyekiti akiweka sharti la kuzuia
kushangilia hata kama wakiguswa. Lakini sharti hilo lilionekana
kuwasumbua wajumbe hao na mara kwa mara wakajikuta wakilipuka na
kushangilia.
Akijinadi kwenye mkutano huo, Dk
Magufuli, ambaye alizungumza kwa dakika tisa kuanzia saa 5:55 hadi saa
6:04 usiku, aliwashukuru wajumbe wa mkutano huo, wakiwamo wageni
waalikwa na muda huo wajumbe wakaanza kumshangilia.
“Naombeni
kura kwa sababu ninaamini kuwa nitafanya kazi na nyinyi na mtanituma na
nitakuwa mwakilishi wenu na nitailinda CCM katika kushinda kikamilifu
na kushika dola ili kuiongoza nchi hii. Nitadumisha Muungano wetu,”
alisema Magufuli.
“CCM
imenilea na ninawaahidi wajumbe sitawaangusha. Nimefanya kazi na Rais
Kikwete na nadhani sikukuangusha. Umenituma katika kipindi chote cha
miaka 10 na nilidhani leo utataka nielezee bar
MWANANCHI
Marais wastaafu watatu na makamu wa
zamani wa CCM jana walifanya kazi kubwa ya kukinusuru chama hicho
kuingia kwenye mgogoro uliokuwa unanukia baada ya Waziri Mkuu wa zamani,
Edward Lowassa kuenguliwa kwenye mbio za urais.
Kwa mara ya kwanza, wajumbe watatu wa
Kamati Kuu ya chama hicho juzi walijitokeza hadharani na kupinga uamuzi
wa chombo hicho wa kupitisha majina ya wagombea kwa njia ambazo walisema
zinazokiuka katiba ya CCM.
Kama hiyo haitoshi, jana wajumbe wa
Halmashauri Kuu walimuweka mwenyekiti wao, Rais Jakaya Kikwete kwenye
hali ngumu baada ya kuimba wimbo wa kuonyesha kuwa na imani na Lowassa,
likiwa ni tukio la kwanza la aina yake kwenye vikao vya juu vya chama na
ambalo liliashiria kuanza kupoteza utii kwa chama.
Habari kutoka ndani ya NEC zinasema kuwa
baada ya mapumziko ya chakula cha mchana, kikao hicho kilijadili kwa
kirefu sakata la kuchujwa kwa Lowassa na pande zinazohusika zilizungumza
kwa hisia kali, ndipo marais hao, Benjamin Mkapa, Ali Hassan Mwinyi,
Abeid Amani Karume na makamu mwenyekiti wa zamani, John Samuel Malecela
walipolazimika kuingilia kati.
“Ilibidi kwanza wote waliokuwa
wanagombea urais waondolewe kwenye mkutano ndipo tuanze kujadiliana,”
alisema mmoja wa wagombea ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe.
Mjumbe mwingine wa kikao hicho alisema
Malecela, Mkapa, Karume na Mwinyi walitumia maneno ya busara na
kuwatahadharisha wajumbe dhidi ya misimamo yao.
“Walituonya kuhusu kujali masuala yetu
binafsi kuliko amani ya nchi na kututaka kuangalia sana misimamo yetu
kwa kuwa inaweza kuhatarisha amani,” alisema mjumbe huyo.
Alisema wakati kikao kilipositishwa kwa
ajili ya chakula cha mchana, kuna baadhi ya wajumbe waliondoka eneo hilo
na wengine kubaki, akiwamo Lowassa ambaye hakujulikana alielekea eneo
gani kwenye jengo hilo.
Kikao cha mchana kilianza bila ya
Lowassa kuwamo na Karume alianza kuzungumza, na kufuatiwa na Malecela,
Mkapa, na Mwinyi, ambaye alipomaliza aliwashauri wajumbe kuwa waendelee
na upigaji kura kwa kuwa suala hilo limeshaeleweka.
Mkutano ulipoanza kupiga kura ndipo
Lowassa alipoingia na kukuta kazi ya upigaji kura inaendelea na hivyo
kuendelea na shughuli hiyo.
Awali, kwa mara ya kwanza, Kikwete jana
alikumbana na mapokezi ya aina yake wakati wajumbe walipomuonyesha
waziwazi kupinga uamuzi wa Kamati Kuu kwa kuimba wimbo wa kumuunga mkono
Edward Lowassa kabla ya kikao cha Halmashauri Kuu kuanza.
Hali hiyo imetokea wakati baadhi ya
wanachama wa CCM wakiwa bado hawajakubali kuenguliwa kwa Lowassa kwenye
kinyang’anyiro cha urais kwa tiketi ya CCM baada ya Kamati Kuu kupitisha
majina ya John Pombe Magufuli, Amina Salum Ali, Bernard Membe, January
Makamba na Dk Asha Rose Migiro kwa ajili ya kupigiwa kura Halmashauri
Kuu.
HABARILEO
Zoezi la uboreshaji daftari la kudumu la wapiga kura kwa mkoa wa Dar es Salaam limesogezwa mbele hadi Julai 22 mwaka huu.
Uamuzi huo umetokana na Tume ya Taifa ya
Uchaguzi (NEC) kupokea maombi kutoka kwa wadau mbalimbali walioomba
tarehe ya kuanza uandikishaji iliyopangwa kufanyika kuanzia Julai 16
iahirishwe ili kupisha sherehe za Eid-El-Fitr ambazo zinatarajiwa
kufanyika kuanzia tarehe hizo.
Taarifa iliyotolewa na Tume ilisema kuwa
kwa kuzingatia umuhimu wa sherehe ya waumini wa dini ya Kiislamu pamoja
na watu wengine Tume imeamua kusogeza tarehe ya kuanza kwa uboreshaji
wa daftari hilo hadi Julai 22.
“Tume imezingatia kwa uzito maombi
yaliyotolewa na wadau mbalimbali kuhusu kusogezwa mbele tarehe ya
uandikishaji uliotakiwa kuanza Julai 16 na badala yake kazi hiyo itaanza
rasmi Julai 22 hadi 31 mwaka huu,” ilisomeka taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa Tume hiyo, uandikishaji
unawahusu wananchi wa mkoa wa Dar es Salaam pamoja na wananchi wa kata
ya Bunju na Mbweni waliojiandikisha wakati wa majaribio.
Aidha Tume inatoa wito kwa wananchi wote
wa mkoa wa Dar es Salaam kujitokeza kwa wingi kujiandikisha ili
wasipoteze haki yao ya msingi ya kidemokrasia.
No comments:
Post a Comment