Friday, July 17, 2015

MWANZA YALAANI MAUWAJI YALIYOFANYWA NA MFANYABIASHARA. J4.


Serikali mkoani Mwanza imelaani mauwaji yaliyofanywa na mfanyabiashara maarufu jijini humo Jumanne Mahende(J4) hivi karibuni katika eneo la Nyakato Sokoni katika Wilaya ya Ilemela mkoani humo.
Tamko hilo limetolewa na mkuu wa mkoa wa Mwanza Magesa Mulongo wakati akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake mapema hivi leo, akitoa tamko hilo mbele ya waandishi wa habari, Mkuu wa mkoa wa Mwanza  amesema sio kitendo kinacho kubalika wala kuhalalishwa na mtu yeyote mwenye roho ya binadamu.
Mulongo amesema, hata wavumilia wala kuwachekea watu wanao thubutu kutoa uhai wa mtu kwa kisingizio cha madeni, “nataka wananchi wafahamu hakuna mbadala wa uhai wa mtu, kama Serikali ya mkoa, wataiomba mahakama iweze kutenda haki pale ambapo ushahidi utakapojitosheleza ili haki ipatikane.
Aidha, amesema hakuna mtu aliye juu ya sheria na kuamua kutoa uhai wa mtu mwingine. ”Ndugu zangu nataka kila mmoja wetu afahamu hakuna mbadala wa maisha au uhai wa mtu, haiwezekani mtu afanye mauwaji halafu aachwe aendelee kutamba kwa kusema yupo karibu na vyombo vya usalama, mimi kama mkuu wa mkoa nataka umma ufahamu kuwa tunataka kuongoza watu kwa amani na utulivu na ikitokea mmoja hataki kufuata utaratibu lazima sheria ifuate mkondo wake.

Alisema  “ kuondoa haki ya mtu kuishi na kufanya wategemezi wa familia kuwa wategemezi kwa watu wengine kitu ambacho kina dumaza uchumi wa mtu mmoja mmoja, jamii lakini uchumi wa mkoa na nchi kwa ujumla.
Wakati huohuo ameiomba jamii ya wanamwanza kutoa ushirikiano wa dhati kwa kutoa taarifa kwa vyombo vya dola pindi wanapo ona kuna viashiria vya uvunjifu wa amani huku akiahidi kusimama kidete na kuona haki inatendeka kikamilifu.

Mbali ya kutoa karipio hilo, mkuu huyo wa mkoa ametumia wasaa huo kutoa taarifa ya uandikishaji wapigakura kwenye daftari la kudumu la wapiga kura kwa mfumo wa BVR katika mkoa huo na kusema mkoa umevuka lengo kwa kufikisha asilimia 103, ambayo ni mafanikio makubwa kutokana na malengo waliyo jiwekea hapo awali.

Alisema  hapo awali mkoa ulijiwekea malengo ya kuandikisha watu 1,403,743 lakini kutokana na maandalizi na mipango mizuri ya mkoa wamefanikiwa kuandikisha watu 1,442,391 sawa na asilimia 103. 

Akitoa mchanganuo huo kwa kila jimbo alisema Jimbo la Nyamagana wameandikisha watu (273,636). Ilemela (234,879), na Sengerema (153,054), majimbo mengine ni Buchosa (158,510), Misungwi (149,535), Magu (147,155),Kwimba (86,273), Sumve (76,466) na Ukerewe (162,883).
Mkoa wa Mwanza kwa mujibu wa Sensa ya watu wa makaazi ya Mwaka 2012 ulikuwa na watu wapatao Mil.2.7.

No comments:

Post a Comment